AfDB yaidhinisha mkopo wa dola milioni 120 ili kugharamia ujenzi wa mradi wa umeme wa maji Tanzania
2020-11-27 19:05:47| CRI

Benki ya Maendeleo ya Afrika AfDB imeidhinisha mkopo wa dola za kimarekani milioni 120 ili kugharamia ujenzi wa mradi wa umeme wa maji kaskazini mwa Tanzania.

Kwenye taarifa yake iliyoitoa jana Alhamis, benki hiyo imesema mradi wa umeme wa maji wa Malagarasi, ambao unagharimu dola za kimarekani milioni 144.14, utatoa umeme wa uhakika majumbani, shuleni, kwenye zahanati na makampuni madogo na ya kati mkoani Kigoma. Mbali na dola milioni 120 zilizotolewa na AfDB na dola milioni 20 za ziada zilizochangiwa na Mfuko wa Ukuaji wa Pamoja wa Afrika (AGTF), serikali ya Tanzania kwa upande wake itatoa kiasi kilichobaki cha fedha dola milioni 4.14.

Kwa mujibu wa taarifa mradi huo unatarajiwa kutoa ajira 700 wakati wa ujenzi wake, na kupunguza gharama za umeme kwa takriban dola 0.04 kilowatt kwa saa, ambazo ni chini kuliko bei ya sasa ya dola 0.33 kilowatt kwa saa.