Serikali ya Ethiopia yasema jeshi la ulinzi limeamriwa kumaliza awamu ya mwisho ya operesheni katika jimbo la Tigray
2020-11-27 08:56:12| CRI

Serikali ya Ethiopia imesema kuwa imeanza awamu ya mwisho ya operesheni ya kijeshi dhidi ya wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi wa Watu wa Tigray (TPLF) kaskazini mwa nchi hiyo.

Wito huo umetolewa na waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, katika taarifa iliyotolewa jana, huku akisisitiza kuwa kipindi cha saa 72 kilichotolewa kwa wahalifu wa TPLF kujisalimisha kimemalizika.

Amesema kuwa jeshi la nchi hiyo limeelekezwa kumaliza awamu ya tatu na ya mwisho ya operesheni ya kurejesha utawala wa sheria, na umakini mkubwa utachukuliwa ili kulinda maisha ya raia wasio na hatia.

Habari nyingine zinasema, ongezeko la wakimbizi wa Ethiopia wanaoingia nchini Sudan limeibua wasiwasi wa kutokea kwa janga la kibinadamu. Hayo yamesemwa na mkuu wa Tume ya Wakimbizi katika mkoa wa Kassala nchini Sudan, Al-Sir Khalid, alipozungumza na Shirika la Habari la China, Xinhua. Amesema hakuna mwitikio wowote kutoka kwa wadau na mashirika ya kibinadamu ya kimataifa kwa mahitaji ya wakimbizi hao, ikiwemo chakula, maji, huduma za afya na makazi.