Rais Mteule wa Marekani Bw. Joe Biden anatarajiwa kumteua mwanasheria mkuu wa jimbo la California Bw. Xavier Becerra kuwa waziri wa Afya na huduma kwa binadamu. Bw. Biden anatarajia kutangaza uteuzi huo hivi karibuni, sambamba na uteuzi wa maofisa wengine waandamizi wa afya, ikiwa ni pamoja na mkuu wa Kituo cha kudhibiti na kupambana na maradhi CDC.
Bw. Becerra alichukua nafasi ya Makamu wa Rais Mteule Bibi Kamala Harris kuwa mwanasheria wa jimbo hilo kabla hajateuliwa kuwa seneta wa jimbo hilo. Kama uteuzi wake ukipitishwa atakuwa ni ofisa muhimu kwenye mapambano dhidi ya COVID-19.
Mtaalamu wa magonjwa ya kuambukizwa na mkuu wa taasisi ya taifa ya magonjwa ya mzio na ya kuambukiza Dr. Antony Fauci, yeye amesema atakuwa mshauri mkuu wa mambo ya afya wa Bw. Biden.