Wanawake Watalikiwa Mara 28 Ili Kuweza Kupata Namba za Usajili wa Gari
2020-12-24 10:30:00| cri

Polisi mjini Beijing imetangaza kutatua kesi moja ya kuhamisha kiharamu namba za usajili wa magari baada ya mwanamke mmoja kukutwa kuwa ametalikiwa mara 28 kwa makusudi ili kupata namba hizo za usajili za mji wa Beijing. Kesi hiyo imezusha mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamiii ya China.

Hiyo ni moja ya kesi 124 zilizolengwa kwenye kampeni maalumu iliyozinduliwa na Polisi mjini Beijing kupambana na uhamishaji haramu wa namba za usajili wa magari kupitia ndoa.

Tangu Oktoba 30, Polisi mjini Beijing wameshirikisha matawi 16 na vikosi 510 vya polisi kwenye juhudi za pamoja za kuvunja mnyororo wa uhalifu huu na wakala haramu wanaohusika.

Kwa mujibu wa Polisi, jumla ya washukiwa 166 wamekamatwa hadi kufikia Ijumaa iliyopita, na 124 kati yao walihusika katika kupata au kununua namba za usajili wa magari za Beijing kwa njia ya utapeli kupitia ndoa.

Kwenye kesi moja ya ajabu iliyotajwa awali, mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 37 aliolewa na kutalikiwa mara 28 na kufanikiwa kuhamisha namba 23 za usajili kupitia ndoa hizo katika miaka miwili iliyopita.

Wanamtandao wa Weibo walieleza kushangazwa na idadi hiyo kubwa ya ndoa alizofunga, na pia walipendekeza serikali ya mji wa Beijing kulegeza sera yake ya kutoa namba za usajili wa magari ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya wakazi wake.