Hoteli yakosea kuweka miadi ya tarehe ya harusi kwa mwaka mmoja mbele
2020-12-16 14:41:36| cri

Novemba 26, Bw. Ren aliweka miadi ya kufanya sherehe ya harusi kwenye jumba la hoteli moja ya mjini Xi’an tarehe 24 mwezi Aprili mwaka kesho. Lakini siku hiyo usiku akaambiwa kuwa jumba hilo tayari limekodishwa. Habari hiyo ilimshtua mno.

Bw. Ren alisema asubuhi ya Novemba 26, yeye, mama yake na mchumba wake walienda kwa pamoja kwenye hoteli hiyo na kusaini mkataba wa kukodi jumba la kufanya sherehe ya harusi, na pia walilipa dhamana ya Yuan 5,000.

Bw. Ren alisema baada ya kusaini mkataba huo, akatoa kadi za mwaliko kwa jamaa na marafiki zake, na siku hiyo alasiri pia alithibitisha tarehe ya harusi na kampuni ya maandalizi na kulipa dhamana. Lakini siku hiyo usiku, alipigiwa simu na meneja wa hoteli akaambiwa kwamba, jumba la kufanya sherehe ya harusi tayari limekodishwa kwa tarehe hiyo, kwa sababu mfanyakazi wa hoteli alikosea kuweka miadi yake kwa mwaka mmoja mbele hadi Aprili 24 mwaka 2022.

Bw. Ren alikataa mapendekezo yaliyotolewa na hoteli ya kuhamisha mahali pa kufanyia sherehe ya harusi kwenye ofisi ya pembeni, au hata kubadilisha tarehe ya kufanya harusi.

Meneja wa hoteli hiyo amekiri makosa ya mfanyakazi wake yaliyosababisha jumba la hoteli kukodishwa mara mbili kwa tarehe moja.

Baada ya mazungumzo ya muda mrefu, Bw. Ren na hoteli bado hawajafikia mwafaka kuhusu suala hilo. Amedai kuwa hoteli inatakiwa kumlipa fidia mara tatu ya dhamana aliyolipa, na endapo watashindwa tena kufikia makubaliano, ataifungulia mashtaka hoteli hiyo ili kulinda maslahi yake halali.