Mzee amzawadia mchuuzi wa matunda nyumba yenye thamani ya Yuan milioni 3
2020-12-24 20:42:39| cri

Mzee mmoja mwenye umri wa miaka 88 anayeishi mjini Shanghai ameamua kumzawadia nyumba yake yenye thamani ya Yuan milioni 3 kwa mmiliki wa duka la matunda lililoko karibu na nyumba yake, baada ya kufariki dunia.

Mzee huyo anayeitwa Ma amekuwa akiishi peke yake baada ya mkewe kufariki dunia miaka kadhaa iliyopita, na mtoto wake aliyekuwa na tatizo la akili pia alifariki ghafla akiwa nyumbani. Kutokana na upweke, kila siku mzee Ma alitembelea duka hilo la matunda na kukaa kidogo na kupiga soga na mmiliki wa duka hilo kijana Xiao You kutoka mkoa wa Henan, na mara kwa mara kijana huyo humsaidia mzee Ma kwenye mambo ya nyumbani, hata alimsaidia Mzee huyo kuandaa mazishi ya mtoto wake.

Siku moja mzee Ma alianguka nyumbani na kupoteza fahamu (kuzirai), na ni kijana Xiao Yao aliyemgundua na kumpeleka hospitali kwa wakati. Xiao You aliwapigia simu ndugu wa mzee huyo kuwajulisha hali yake, lakini walimwambia kuwa hawana nafasi ya kumuuguza, na Xiao akachukua jukumu hilo mwenyewe. Wakati wa mchana, Xiao alikaa dukani kuendesha biashara yake, na wakati wa usiku alienda hospitali kumhudumia mzee Ma mpaka alipopona na kurudi nyumbani.

Mzee Ma tayari amemchukulia Bw. Xiao Yu kuwa mwanafamilia wa kutegemewa. Baada ya kuruhusiwa kutoka hospitali, Mzee Ma alimwalika Bw. Xiao You na familia yake kuishi pamoja naye na kuunda familia moja maalumu, na mzee Ma akaanza kuhisi furaha ndani ya familia ambayo aliikosa kwa miaka mingi. Baadaye Mzee Ma na Bw. Xiao You walienda pamoja kwenye Ofisi ya Mthibitishaji na kumfanya Bw. Xiao You kuwa mwangalizi wake rasmi, na kuamua kuwa Xiao You atarithi mali zake zote baada ya mzee Ma kufariki.