Vifaa 3,500 vya kushtua moyo (AED) vyawekwa kwenye sehemu za umma mjini Shenzhen
2020-12-25 15:49:00| cri

Kifaa cha AED ambacho ni kifaa-tiba kinachotumia umeme kurudisha mapigo ya moyo katika mwendo wa kawaida hivi karibuni kimesaidia kuokoa maisha ya mtu mwingine mmoja mjini Shenzhen.

Novemba 28 jioni, kijana mmoja mwenye umri wa miaka 26 alianguka ghalfa na kupoteza fahamu wakati akiendesha baiskeli. Baada ya kupigiwa simu ya dharura kuhitaji msaada, daktari na wauguzi wa kituo cha afya cha karibu walifika mara moja wakiwa na kifaa cha AED, na kufanikiwa kuokoa maisha ya kijana huyo.

Mkurugenzi wa Kitengo cha Dharura cha Hospitali ya Luohuo mjini Shenzhou Wang Lanxiang amesema, bila ya kifaa cha AED, isingekuwa rahisi kuokoa maisha ya kijana huyo aliyekumbwa na mshtuko wa moyo. Ameongeza kuwa kama wagonjwa wa mshtuko wa moyo wakiweza kupewa msaada wa kwanza wa CPR ndani ya dakika nne, kutakuwa na uwekezano wa asilimia 50 wa kuokoa maisha wao, muda huo kitaaluma unaitwa “Dakika Nne za Dhahabu”. Kama kifaa cha AED kikitumiwa wakati wa msaada wa kwanza, uwekezano wa kuokoa maisha unaweza kufikia asilimia 90.

Kifaa cha AED ni kifaa cha kuokoa maisha kinachoweza kutumiwa kirahisi, na kwa kupewa mafunzo mafupi, kila mtu anaweza kukitumia vizuri.

Imefahamika kuwa mwaka 2017, mji wa Shenzhou ulizindua mpango wa kuweka vifaa vya AED kwenye sehemu za umma. Hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu, vifaa 3,500 vya AED vilivyonunuliwa na serikali ya Shenzhou vyote vimewekwa kwenye maeneo ya umma.