China ni nchi pekee iliyofanikiwa kutimiza malengo ya mapambano dhidi ya umaskini kwa mwaka 2020
2020-12-29 09:03:13| cri

Mwaka 2015 serikali kuu ya China ilitangaza kuwa mtu yoyote mwenye kipato cha chini ya Yuan 2,800 kwa mwaka (yaani dola za Marekani 427) basi mtu huyo alitajwa kuwa anaishi chini ya mstari wa umaskini, kigezo hicho kiliinuliwa kutoka Yuan 2,300 kwa mwaka, kilichowekwa mwaka 2011. Kigezo hiki cha China ni tofauti na kile kinachofuatwa na benki ya dunia, sababu ni kuwa kuna tofauti kubwa ya kiuchumi, kimazingira na hali ya maisha, kati ya China na nchi nyingine duniani.

 

Mwaka 2015 wakati serikali imeweka kigezo cha Yuan 2800 kuwa mstari wa umaskini, maeneo 14 ya China hasa yaliyoko milimani ndio yaliyotajwa kuwa yanakabiliwa zaidi ya hali ya umaskini. Serikali kuu imekuwa na lengo la kutokomeza umaskini tangu ilipoanza kutekeleza sera ya mageuzi na kufungua mlango. Lakini ni kuanzia mwaka 2013, ambapo idadi ya watu wanaoishi kwenye umaskini mkali ilianza kupungua kwa kasi.

 

China imekuwa ikitumia njia mbalimbali kupambana na umaskini, moja imekuwa ni kuendeleza sekta mbalimbali kama vile utalii, biashara kwa njia ya mtandao wa internet. Pia imekuwa ikitekeleza miradi mingi ya kuwahamisha watu wanaoishi kwenye mazingira magumu kijiografia na kuwafanya waishi maeneo bora zaidi bila kusumbuliwa na majanga ya asili kama matetemeko ya ardhi, mafuriko, maporomoko ya udongo, na kumekuwa na programu maalum za kuboresha sekta za afya, elimu na huduma mbalimbali za kijamii.

 

Pamoja na kuwa watu wengi wanahusisha suala la kupambana na umaskini na kipato, yaani dola 427 kwa mwezi. Ukweli ni kwamba kipato ni moja tu ya vigezo kati ya vigezo mbalimbali vinavyotazamwa na China kwenye kupambana na umaskini. Kwa ujumla vita ya kupambana na umaskini inaangalia mambo ya elimu, afya, chakula, makazi, huduma za jamii, na hata miundo mbinu. Katika kipindi cha miaka 40 iliyopita, China imekuwa na maendeleo makubwa katika maeneo yote hayo, na wakati inatangaza ushindi kwenye vita dhidi ya umaskini, ushindi mkubwa zaidi upo kwenye sekta mbalimbali.