Idadi ya wanafunzi wa kike yazidi nusu ya idadi ya jumla ya wanafunzi wa elimu ya juu wa China
2020-12-30 15:09:12| cri

Ripoti iliyotolewa hivi karibuni na Idara ya Takwimu ya China kuhusu Mwongozo wa Maendeleo ya Wanawake wa China kati ya mwaka 2011 na 2020, imeonesha kuwa mfumo wa huduma ya afya ya akina mama wa China umekuwa ukikamilika zaidi, na kazi ya kuondoa pengo la kijinsia katika kipindi cha elimu ya lazima imefanyika, na idadi ya wanawake walioajiriwa inaendelea kuzidi kiwango cha asilimia 40. Ripoti hiyo pia imeonesha kuwa idadi ya wanafunzi wa kike wenye elimu ya juu inazidi nusu ya ile ya jumla ya wanafunzi wote. Katika miaka ya hivi karibuni, elimu ya juu ya China imepata maendeleo ya kasi, na kiwango cha jumla cha uandikishaji wa wanafunzi wanaosoma elimu ya juu kimeongezeka haraka kutoka asilimia 26.5 ya mwaka 2010 hadi asilimia 51.6 ya mwaka 2019.

Mwaka 2019, idadi ya wanafunzi wenye elimu ya juu ilikuwa milioni 1.45 katika vyuo vikuu, ambayo inachukua asilimia 50.6 ya ile ya jumla ya wanafunzi wa elimu ya juu, na ongezeko limefikia asilimia 2.7 ikilinganishwa na mwaka 2010.

Mbali na hayo, idadi ya wanawake walioajiriwa imeendelea kuzidi kiwango cha asilimia 40. Mwaka 2019, Wizara ya Rasilimali Watu na Huduma za Jamii ilitangaza waraka ukifafanua vitendo vya aina sita vya ubaguzi wa kijinsia katika mambo ya ajira ambavyo havipaswi kutekelezwa, ili kuhakikisha wanawake wanapewa fursa sawa kwenye ajira.

Mwaka 2019 idadi ya waajiriwa wa kike kote nchini ilikuwa imefikia asilimia 43.2, na idadi ya wanawake walioajiriwa mijini ilikuwa imefikia milioni 66.842, ikiongezeka kwa asilimia 37.5 kuliko mwaka 2010.