Kuimarika kwa uchumi wa China kunatoa matumaini kwa ulimwengu hasa mataifa yanayoendelea
2020-12-31 08:27:27| cri

Na Eric Biegon

Janga la virusi vya Corona lilitoa changamoto kubwa kwa uchumi wa China. Taifa hilo lilisimamisha kila aina ya shughuli katika robo ya kwanza ya mwaka 2020 ili kuzuia kuenea kwa virusi hivyo, maduka ya rejareja yalifungwa, na viwanda vikafungwa. Lakini baada ya kufanikiwa kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo kwa kiwango kikubwa katika robo ya pili ya mwaka 2020, uchumi wa China umeanza yena kuimarika, ikiwa ni kinyume na matarajio ya wengi.
Kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni kutoka Benki ya Dunia, mafanikio hayo yamewezeshwa na mikakati mahsusi ya kudhibiti janga na sera madhubuti. Katika ripoti hiyo, Benki hiyo imekadiria kuwa uchumi wa China utaongezeka hadi asilimia 7.9 mwaka ujao, ikiwa ni juu zaidi ya nchi nyingine duniani.
Kutokana na ripoti hiyo, wataalamu wanasema serikali ya China imedhihirisha uwezo wa kuimarisha uchumi wake japo kuna shinikizo la ndani na nje ya nchi.
Kwa Kenya, ukuaji huu una maana kubwa, hasa katika suala la kufikia malengo ya kitaifa kama vile kupunguza umaskini, ambapo China imefanikiwa kuondoa kaunti zote kutoka kwenye orodha ya umaskini. Hivi karibuni serikali ya China ilitangaza kwamba, kaunti tisa za mwisho zilizokuwa kwenye umasikini uliokithiri kusini magharibi mwa nchi hiyo, zimeondokana na umaskini kamili. Nitajadili umuhimu wa hatua hii baadaye.
Kwa mataifa ya nje, ujumbe mkubwa unaotolewa na mtazamo huu kwa washirika wa China kibiashara ni kwamba, uchumi wa nchi hiyo bado umeendelea kuwa imara. Na hii ni muhimu kwani tukifuatilia hali ilivyo duniani hivi sasa, taarifa za migogoro ya kibiashara na kuhujumu ushirikiano wa kimataifa zimekuwa zikigonga vichwa vya habari.
Wakati haya yakiendelea, China inashikilia ushirikiano wake na ulimwengu wote, hasa kuimarisha uhusiano na mataifa yanayoendelea, hivyo kuimarika kwa uchumi wa China kunatoa matumaini zaidi kwamba uhusiano huu haukabiliwi na tishio lolote.
Kuimarika kwa uchumi pia ni muhimu katika uratibishwaji wa sera za nje za China, na katika miaka michache yaliyopita, nchi hiyo ya pili kiuchumi duniani imekuwa ikitetea maadili ya pamoja. Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja lililotolewa na rais Xi Jinping wa China, ni mfano halisi. Kupitia Pendekezo hilo, dhamira ya rais Xi ni kujenga "jamii ya binadamu yenye mustakabali wa pamoja". Kupitia mpango huu, China imetoa zaidi ya dola za Marekani trilioni 4 katika miaka saba iliyopita pekee, ambapo takriban miradi 3,200 imejengwa kote duniani.
Barani Afrika, China kwa sasa ni mfadhili mkubwa wa miradi ya miundombinu, mingi imekamilika, na mingine inaendelea na miradi mingi zaidi imepangwa. Miradi hii inaweza tu kuendelezwa ikiwa misingi ya kiuchumi ya Beijing yatabaki imara.
Umuhimu wa Pendekezo la ‘Ukanda Mmoja, Njia Moja’ kwa Afrika ni wazi kwa wote, kwani hadi sasa nchi 42 za Afrika zimejiunga na pendekezo hilo. Huu ni ushuhuda tosha kwamba mataifa mengi ya Afrika yanaona haja ya miundombinu bora, ambayo bado inaonekana kama kikwazo kikubwa cha maendeleo katika eneo hilo.
Baadhi ya miradi ambayo imekamilika chini ya Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja, ni pamoja na barabara kuu ya Cherchell Ring Expressway nchini Algeria, reli inayounganisha Addis-Ababa na Djibouti, Bandari ya Doraleh nchini Ethiopia, reli ya Mombasa-Nairobi ya Kenya, Daraja la Maputo-Katembe nchini Msumbiji, reli ya Lagos-Kano nchini Nigeria, na barabara kuu inayounganisha uwanja wa ndege wa Entebbe na mji wa Kampala nchini Uganda.
Ni muhimu kusema kuwa, uwekezaji wa China barani Afrika umeongezeka kwa kiasi kikubwa tangu pendekezo hilo lilipozinduliwa. Ripoti ya hivi karibuni ya kampuni ya McKinsey inakadiria kuwa, zaidi ya makampuni 10,000 ya China yanafanya kazi barani Afrika, na ripoti mbalimbali zinaonyesha uwekezaji huu umekuwa na matokeo mazuri barani humo.
Nchini Kenya, ujenzi wa barabara kuu inayounganisha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta na sehemu za Magharibi mwa Nairobi unaendelea, na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa 2021. Miradi hii michache ni baadhi ya maendeleo ya miundombinu inayojengwa kote barani, na inatoa fursa kubwa za uwekezaji.
Mambo haya yanafanyika wakati China imefichua kwamba tayari imetoa robo tatu ya ahadi ya fedha iliyotolewa kwa Afrika mwaka 2018. Waziri msaidizi wa Mambo ya Nje wa China Deng Li amesema, zaidi ya asilimia 70 ya dola za Marekani bilioni 60 za msaada wa kifedha ulioahidiwa na China katika Mkutano wa FOCAC uliofanyika Beijing tayari zimewasilishwa au kupangwa kutolewa.
Kutokana na hali nzuri ya uchumi, Bw. Deng alibainisha kuwa China itatafuta njia mpya ya ushirikiano na Afrika inayolenga miradi ambayo itabadilisha hali ya maisha ya watu. Amesema China ina hamu ya kushiriki miradi ambayo "inazalisha mamilioni ya ajira, kuboresha maisha, kukuza uchumi wa kidijitali, kupunguza umaskini, na kuimarisha sekta ya viwanda."
Nikirejelea umuhimu wa ukuaji huu wa uchumi kwa Kenya, China kwa sasa inabadili mwenendo na kuwa na uchumi unaoendeshwa na soko. Uamuzi huu utahakikisha kuwa China inaongeza manunuzi yake ya bidhaa zinazoagizwa kutoka nje.
Huku ikiwa na watu bilioni 1.4, China inajivunia asilimia 20 ya idadi ya watu duniani, na raia wake wanapoinuka kiuchumi, pia matumizi yao yanaongezeka, na makampuni yatajitahidi kuuza bidhaa zao kwenye soko hili, ambalo ni kubwa zaidi duniani. Nchi nyingi zinazoendelea bado ni wazalishaji wakuu wa bidhaa za kilimo na maliasili, na kuongezeka kwa mahitaji ya bidhaa hizi nchini China kutaboresha bei za bidhaa hizo.
Hivi sasa Afrika inahitaji kichocheo cha ukuaji, na kupitia kuendelezwa kwa sera imara ya kiuchumi, China inaweza kutoa msukumo huo kwa ukuaji wa uchumi wake. Lakini je, unafahamu kuwa uchumi wa China unaelekea kuwa namba moja duniani katika miaka 8 ijayo?
Ripoti iliyotolewa na Kituo cha Utafiti wa Uchumi na Biashara CEBR inasema, uchumi wa China utashinda uchumi wa Marekani itakapofika mwaka 2028, miaka mitano kabla ya utabiri wa awali, kutokana na mgogoro wa uchumi unaosababishwa na janga la Corona.
CEBR inasema, kando na China kushughulikia janga hilo kwa ufanisi zaidi kuliko mataifa ya Magharibi, athari za ukuaji wa uchumi kwa nchi hizo zitadumu kwa muda mrefu.