Tanzania yajipanga kuongeza bidhaa nyingi zaidi katika soko la China
2021-01-07 18:55:35| cri

Serikali ya Tanzania imesema imejipanga kuzalisha bidhaa nyingi zaidi na zenye ubora unaokidhi soko la kimataifa ili kuongeza bidhaa zake katika soko la China.

Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki,Profesa Palamagamba Kabudi,akizungumzia ujio wa Waziri wa Mambo ya nje wa China,Wang Yi,alisema biashara kati ya Tanzania na China imekuwa ya mafanikio makubwa na Tanzania imejipanga kuongeza bidhaa zake katika soko la China.

Takwimu za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki zilizotolewa katika taarifa fupi kuhusu Tanzania na China mwishoni mwa mwaka jana,zinaonesha kuwa,katika kipindi cha miaka mitano  (2014-2018) mauzo ya bidhaa za Tanzania katika soko la China yamefikia wastani wa dola U$145milioni kwa mwaka.

Aidha ,katika kipindi hicho serikali imefungua fursa mpya za kuuza bidhaa mbalimbali katika soko la China ikiwemo zao la muhogo,mazao ya baharini,mabondo ya samaki,pembe za ng’ombe ,mashudu na maharage ya soya.

Profesa Kabudi alisema pamoja na mafanikio yaliyopatikana bado kuna changamoto ya urari wa biashara ambapo China inauza zaidi bidhaa nchini Tanzania kuliko Tanzania inavyouza bidhaa katika soko la China.

Alisema kuwa ziara ya Wang itagusia suala hilo.