Vijana wapewa fursa ufugaji samaki wa mabwawa
2021-01-08 16:35:44| cri

Serikali ya Tanzania imewataka vijana kujihusisha na ufugaji wa samaki katika mabwawa ili kuwaokoa na kilio cha ukosefu wa ajira nchini.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi wa Tanzania Pauline Gekul aliyasema hayo alipotembelea kampuni ya ufugaji wa samaki ya Big fish, wilayani Kigamboni, jijini Dar es Salaam.

Alisema mwelekeo wa serikali kwa sasa ni kuimarisha ufugaji wa samaki katika mabwawa kwa kuwa uvuvi wa kutegemea maji ya asili umekuwa mkubwa na kusababisha kupungua kwa rasilimali za uvuvi lakini kimbilio pekee litakalowawezesha vijana wengi kupata ajira ni ufugaji wa samaki katika mabwawa.

Aliongeza kuwa serikali ipo mbioni kuweka miongozo na kanuni za ufugaji huo ili kuwalinda na kuwawezesha wafugaji kufuga vizuri na kwa kuzingatia taratibu zitakazowekwa. VKauli hiyo inakuja wakati ambapo rais wa Tanzania John Magufuli ameahidi ajira zaidi ya milioni nane, moja ya sekta ambayo inategemewa kutengeneza ajira hizo ni ya uvuvi. Vijana nchini humo wamekuwa wakihimizwa kuchangamkia fursa hiyo ya uvuvi ili waweze kujikomboa kiuchumi.