Tanzania kuwabana walaji fedha za ushirika
2021-01-08 16:34:13| cri

Serikali ya Tanzania imeapa kutocheka na mtu yeyote atakayebainika kuchezea fedha za ushirika ikiwa ni juhudi za kurudisha hadhi na heshima ya ushirika.

Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda amesema wanatarajia kuitisha mkutano wa wadau wa ushirika ili kupitia upya Sheria ya Ushirika iliyopo ili iendane na mahitaji ya sasa.

Mkenda alisdema hayo katika hafla ya kukabidhi magari matano na kompyuta 70 kwa ajili ya kurahisisha utendaji kazi kwa watumishi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC).

Alisema bado kunahitajika mapambano dhidi ya wizi na ubadhirifu kwenye vyama vya ushirika licha ya kuonekana kupungua kutokana na jitihada zilizofanywa na serikali za kurudisha mali za ushirika. Alisema kuwa licha ya ubadhirifu kupungua, bado kuna tatizo la vyama kushindwa kuandaa vyema hesabu zake na kusababisha kukosa hati safi.

Alinukuu ripoti ya ukaguzi wa vyama vya ushirika 43 iliyofanywa na Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) kwa mwaka 2019/20, inayoonyesha hakuna chama kilichopata hati safi.