RAGA: Timu ya Shujaa yapangiwa mechi zaidi za kirafiki barani Ulaya
2021-01-08 15:34:50| cri

Wachezaji wa timu ya taifa ya Raga nchini Kenya, Shujaa, wamepangiwa mechi tatu za ziada za kirafiki kwa ajili ya kujifua kwa Michezo ya Olimpiki itakayoandaliwa jijini Tokyo, Japan kuanzia Julai 2021. Kikosi hicho tayari kimeratibiwa kupimana nguvu na Ufaransa na Uhispania katika mechi zitakazochezwa Februari 2021. Wakiwa katika mataifa hayo, Shujaa watavaana pia na vikosi vya New Zealand, Afrika Kusini, Australia, Fiji na Samoa. Kwa mujibu wa meneja wa timu ya Shujaa, Eric Ogweno, Shirikisho la Raga Duniani (WR) limepania kuvipa vikosi ambavyo tayari vimefuzu kwa Olimpiki fursa nyingi za kujifua vilivyo kwa mashindano hayo makubwa.