RIADHA: Uwanja wa Nyayo kutumika katika duru zote tatu za mbio za kupokezana vijiti za AK
2021-01-08 15:34:20| cri

Duru zote tatu za Mbio za Kupokezana Vijiti za Shirikisho la Riadha la Kenya (AK) zitaandaliwa katika uwanja wa Nyayo, Nairobi. Kwa mujibu wa mkurugenzi wa mashindano katika Shirikisho hilo, Paul Mutwii, imekuwa vigumu kwa shirikisho kuandaa mapambano makubwa nje ya Nairobi kwa sababu ya changamoto za kudhibiti maambukizi ya virusi vya Corona. Awali, Nairobi ilitarajiwa kuwa mwenyeji wa duru ya kwanza itakayofanyika kesho Januari 9, huku duru ya pili ikitarajiwa kufanyika katika eneo la North Rift Januari 23. Uwanja wa Kericho Green ulikuwa uwe mwenyeji wa duru ya tatu mnamo Februari 6 kabla ya mchujo wa kitaifa kwa minajili ya kufuzu kwa Mbio za Dunia za Kupokezaka Vijiti kufanyika kati ya Machi 26-27 ugani Nyayo. Mbio za Dunia za Kupokezana Vijiti zimepangwa kufanyika mjini Selesia, Poland kuanzia tarehe 1-2, Mei, 2021.