SOKA: Frank Lampard akabiliwa na wakati mgumu Stamford Bridge
2021-01-11 17:04:38| CRI

Kimekuwa ni kipindi kigumu kwa Frank Lampard. Kwani yeye mwenyewe amethibitisha kwamba kibarua chake kipo kwenye mstari mwekundu ikiwa matokeo mabaya yataendelea kutawala kwenye ubao wa Stamford Bridge. Lampard ambaye ameshuhudia kikosi chake kikicheza mechi tatu mfululizo bila ya kupata ushindi yupo kwenye presha kubwa ya kupoteza kibarua chake na makocha wanaopewa nafasi kubwa ya kuchukuwa mikoba yake ni Ralph Hassenhuttl, Julian Nagelsmann na Thomas Tuchel.

Taarifa zinadai mabosi wa Chelsea wamempa mchezo mmoja ambao ni dhidi ya Fulham, Ijumaa ya wiki hii, ikiwa atapoteza basi ndio itakuwa mwisho wa safari yake. Hata hivyo, Mtendaji Mkuu wa wababe hao Marina Granovskaia ameonyesha kumsapoti zaidi kocha huyo na kumlinda katika kipindi hiki kigumu. Ikumbukwe Lampard alifanya vizuri sana wakati anapewa timu Julai 4, 2019 ikiwa kwenye katazo la kusajili na akaamua kuuchukuwa mzigo huo wa kuni zenye miba bila ya kujali kuchomwa hadi akaiongoza kumaliza nafasi ya nne.