SOKA: Ni nani atakayetua Simba kati ya Jean-Florent Ibengé na Rene Wailer?
2021-01-11 17:03:26| CRI

Si mara ya kwanza jina la Jean-Florent Ibengé kutajwa kwenye soka ya Tanzania, safari hii anahusishwa kuinoa Simba baada ya kuondoka kwa Kocha Sven Vandenbroeck, raia wa Ubelgiji. Ibenge ambaye ni Kocha wa Timu ya Taifa ya DR Congo na Klabu ya AS Vita ya nchini humo, awali alikuwa akihusishwa na Yanga kabla ya ujio wa Cedric Kaze anayeinoa timu hiyo kwa sasa.

Hivi karibuni, Sven aliondoka ghafla kwenye kikosi cha Simba na kuelekea Morocco kabla ya uongozi wa timu hiyo kutoa tamko la kuachana naye ikiwa ni muda mchache baada ya kuifikisha timu hiyo hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu. Taarifa kutoka ndani ya Simba, zinasema kwamba, Ibenge ameibua mvutano ndani ya klabu hiyo kutokana na baadhi ya viongozi kumhitaji, huku wengine wakimtaka Kocha Rene Wailer aliyewahi kuinoa Al Ahly.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba, kimesema kuwa viongozi wengi wa timu hiyo mawazo yao yapo kwa Ibenge kutokana na historia yake nzuri kwenye mashindano ya kimataifa ikiwemo Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo Simba wametinga hatua ya makundi na wanataka kufanya kweli awamu hii.