KIKAPU: Kenya Morans kuingia kambini kwa maandalizi ya kufuzu kombe la AfroBasket
2021-01-11 17:02:54| CRI

Timu ya Kenya Morans itaripoti kambini leo Januari 11 kujiandaa kwa duru ya kufa na kupona ya kuingia Kombe la Afrika la mpira wa vikapu la wanaume (AfroBasket) itakayoandaliwa Februari 19-21, 2021.

Viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Vikapu Kenya (KBF) walikutana Januari 9 na kuamua tarehe hiyo na kuongeza kuwa Morans itafanyiwa vipimo vya kwanza vya virusi vya corona mnamo Januari 13 kabla ya kuzamia maandalizi Januari 15 uwanjani Nyayo.

Morans, ambayo ilivuna medali ya fedha kwenye Kombe la Afrika la wachezaji wanaocheza barani Afrika (AfroCan) mwaka 2019, itapimwa virusi hivyo mara tatu kabla ya kurudiana na Senegal, Angola na Msumbiji katika mechi za Kundi B.

Timu hizi zilimenyana katika duru ya kwanza Novemba 2020 ambapo Morans ilipoteza dhidi ya Senegal na Angola na kubwaga Msumbiji.

Wachezaji 10 wanaocheza mpira wa vikapu nchini Kenya watakuwa katika kundi la kwanza litakaloanza mazoezi. Wachezaji hao wanatarajiwa kutoka kikosi kilichochaguliwa kwa majukumu ya duru ya kwanza, ingawa kocha Cliff Owuor yuko huru kufanya mabadiliko.