Timu ya Taifa stars ya Tanzania kucheza na DRC leo mchezo wa kirafiki
2021-01-12 17:04:09| cri

TIMU ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ inatarajiwa kucheza leo mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya DR Congo kwenye uwanja wa Benjamini Mkapa. Mchezo huo utakaochezwa kuanzia saa 11:00 jioni ni muhimu kwa wote wawili kama kipimo kwa maandalizi ya mwisho ya vikosi vyao kuelekea katika fainali za Mtaifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (Chan) zitakazofanyika Cameroon kuanzia Januari 16, mwaka huu. Kocha Msaidizi wa Stars, Juma Mgunda alisema maandalizi ya wachezaji wake yanatia moyo, hivyo anaamini watafanya kile ambacho wameelekezwa. Alisema watakachofanya ndicho watakachokwenda kuwakilisha katika michuano hiyo mikubwa. Mgunda alitaja mchezaji atakayekosekana ni Dikson Job baada ya kuumia paja. Pia amesema mchezo huo sio tu utaonesha maandalizi yao bali utawafanya watambue mapungufu yao kama yatakuwepo na ikiwezekana kuyafanyia kazi mapema kwa lengo la kufanya vizuri zaidi, kwani wamedhamiria kwenda kushindana na sio kushiriki tu.