SOKA: Manchester United yawa vinara wa ligi kuu Uingereza
2021-01-13 17:58:49| cri

Klabu ya soka ya Manchester United ya nchini Uingereza, imeibuka na ushindi wa goli 1-0 dhidi ya Burnley kwenye mchezo wa ligi kuu nchini humo uliopigwa usiku wa kuamkia leo Januari 13, 2021. Baada ya ushindi huo ambao goli pekee lilifungwa na Paul Pogba dakika ya 71, Manchester United sasa imefikisha pointi 37 na kukaa juu ya msimamo ikiwazidi Liverpool ambao wana pointi 33, baada ya timu zote mbili kucheza mechi 17 mpaka sasa.

Hii ni mara ya kwanza Manchester United kuongoza ligi kuu ya Uingereza baada ya kuwa imecheza mechi nyingi (17), ambapo mara ya mwisho kuongoza ligi baada ya mechi nyingi ilikuwa ni siku ya mwisho ya msimu wa 2012-13 walipotwaa ubingwa chini ya Sir Alex Ferguson. Hata hivyo mbio za ubingwa ndio kwanza mbichi kutokana na ushindani ambao upo msimu huu ambapo vilabu vingi vimekuwa vikisuasua.

Katika ligi ya msimu huu nchini Uingreza karibu timu sita zimeshakaa kwenye usukani wa ligi ya nchi hiyo mpaka sasa ambazo ni Manchester United, Southampton, Aston Villa, Liverpool, Tottenham na Everton.