China yahimiza utekelezaji wa Ajenda ya Mwaka 2030 ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa
2021-01-13 17:06:10| CRI

Waraka wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Maendeleo wa China uliotolewa hivi karibuni na ofisi ya habari ya Baraza la Serikali la China unasema, China imechangia kuhimiza utekelezaji wa Ajenda ya Mwaka 2030 ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa, kupitia kuziunga mkono nchi nyingine zinazoendelea kupambana na umaskini, na kuinua kiwango cha maendeleo ya kilimo, elimu, miundombinu na viwanda.

Ajenda ya Mwaka 2030 ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa ilipitishwa tarehe 25 Septemba mwaka 2015 kwenye mkutano wa kilele wa maendeleo wa umoja huo, ili kuelekeza maendeleo ya nchi mbalimbali duniani na ushirikiano kati yao katika miaka 15 ijayo. Kwa mujibu wa Waraka wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Maendeleo wa China, China imechangia utekelezaji wa ajenda hiyo kwa kuchukua hatua nyingi, ikiwa ni pamoja na kuanzisha miradi ya kielelezo ya ushirikiano wa kupambana na umaskini nchini Laos, Myanmar, Cambodia na nyinginezo, kutuma vikundi vya watalaamu wa kilimo katika nchi za Asia na Afrika, kujenga shule katika nchi zikiwemo Nepal, Msumbiji, na Namibia, na kujenga miradi ya umeme nchini Cuba na Kirgyzstan. Naibu mkuu wa idara ya maendeleo vijijini ya wizara ya kilimo na misitu ya Laos Bounchanh Kombounyasith anasema,

“Mafanikio ya China katika kupunguza umaskini yana maana muhimu ya kuigwa na Laos. Tumeiga na kueneza uzoefu wa China kote nchini kwetu. Mradi wa kielelezo wa ushirikiano kati yetu wa kupunguza umaskini umeleta hali mpya katika vijiji vyetu vitatu, na umekuwa mfano wetu wa kuigwa katika juhudi za kuondoa umaskini vijijini.”

Aidha, China pia imetekeleza miradi mingi ya miundombinu katika nchi zinazoendelea, na kuwaletea watu wa nchi hizo manufaa halisi. Waraka huo unaonesha kuwa, China imezisaidia Sierra Leone, Burundi, Serbia na nchi nyingine kujenga na kukarabati barabara muhimu, na kutoa msaada wa mabasi 100 nchini Syria. Kutokana na mradi wa ujenzi wa jengo jipya la bunge nchini Zimbabwe, wenyeji wengi walipata ufundi stadi. Mkuu wa mradi huo Cai Libo anasema,

“Wafanyakazi wa China na wenyeji ni moja kwa tano. Wachina wanawafundisha wenyeji, ambao baada ya kupata ufundi stadi, watawafundisha wenyeji wengine.”

Waraka huo unasema China itafuata wazo la kuzingatia zaidi watu, na kuendelea kushirikiana na nchi nyingine zinazoendelea kukabiliana na changamoto za kimataifa.