MIELEKEA: Timu ya taifa kuingia kambini wakiwa na wakufunzi wanne
2021-01-13 17:59:16| cri

Shirikisho la Mieleka nchini Tanzania limewaita makocha wanne kuinoa timu ya Taifa inayojiandaa na mashindano ya kufuzu Olimpiki yatakayoanza Aprili 2 hadi 4 na baadaye kuunganisha mashindano ya Afrika kuanzia Aprili 6 hadi 11 nchini Morocco. Michezo ya Olimpiki itaanza mwishoni mwa Julai mwaka huu nchini Japan, Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi shiriki. Katibu mkuu wa Shirikisho la Mieleka, Abraham Ngabuka amesema timu itaanza kambi leo Januari 13 kwenye ukumbi wa Msasani Beach Club. Ngabuka amesema timu hiyo itakuwa na wachezaji 25, ingawa sita kati yao ndiyo wataiwakilisha nchi kwenye mashindano ya kufuzu Olimpiki. Amesema katika kambi hiyo ya wazi, kikosi cha taifa kitanolewa na makocha wanne wakiongozwa na yeye ambaye ndiye kocha mkuu. Amewataja makocha wasaidizi kuwa ni Mwene Mwangwale, Daniel Lyaga na Faraji Katonga. Ngabuka amesema watakuwa na ratiba ya mazoezi kila siku saa 12 Asubuhi hadi saa 4 Asubuhi. Mieleka ni miongoni mwa michezo sita inayopewa nafasi ya kuiwakilisha Tanzania, mingine ni ngumi, judo, riadha, wavu ya ufukweni na kuogelea.