Kenya-Bodi za vyama vya ushirika kahawa kuvunjwa
2021-01-14 19:27:27| cri

Waziri wa Kilimo nchini Kenya Peter Munya ametoa onyo kwa wanachama wa vyama vya ushirika wanaowanyima wakulima haki yao ya kunufaika na pesa za hazina ya kahawa.

Alisema kuwa bodi za vyama vya ushirika zinazofanya hivyo zitavunjwa.

Wakulima wengi wamekuwa wakilalamika kuwa wasimamizi wa vyama vya ushirika wanawanyima pesa kutoka hazina hiyo iliyotengewa Sh.3 bilioni na serikali ya kitaifa.

Waziri Munya amesema pesa zilizotengewa hazina hiyo kwa lengo la kufufua sekta ya kahawa zingali benki kwa sababu wakulima hawajatuma maombi. Bw Munya alisema kwamba bodi za vyama vya ushirika zinadaganya wakulima kwamba wakikopa kutoka hazina hiyo, watakuwa wamepatia kampuni ya New Kenya Planters Cooperative Union (KPCU) haki za kusaga kahawa yao.

Hazina hiyo ilianzishwa na Rais Uhuru Kenyatta kwa lengo la kukinga wakulima wasipate hasara baada ya kuvuna zao lao. Bw Munya waliwahimiza wakulima kuchukua mikopo kutoka hazina hiyo kwa kuwa inatoza riba ya asilimia tatu pekee.