SOKA: Yanga yaibuka kidedea kombe la Mapinduzi
2021-01-14 18:27:00| cri

Kikosi cha Yanga kimeibuka na ubingwa wa Kombe la Mapinduzi baada ya ushindi wa penalti 4-3 dhidi ya Simba baada ya dakika 90 kukamilika kwa sare ya kufungana. Nyota wa mchezo huo ni Farouk Shikalo ambaye aliokoa penalti moja ya Joash Onyango na Meddie Kagere kugongengesha mwamba penalti yake moja.

Saido Ntibanzokiza ambaye alikuwa msumbufu ndani ya dakika zote 90 amesema kuwa wachezaji wenzake walimuomba awape sapoti naye akasema kwamba hana tatizo atafanya kazi. Alifunga penalti ya mwisho iliyomshinda mlinda mlango Beno Kakolanya ambaye hakuwa na namna baada ya kuokoa hatari tano ndani ya dakika 90.

Huu unakuwa ni ubingwa wa pili kwa Yanga inayonolewa na Kocha Mkuu, Cedric Kaze huku Simba ikibakiwa na mataji yake matatu ndani ya kabati lao.