SOKA: Hatimaye kipofu kaona mwezi Sheffield United yashinda kwa mara ya kwanza Ligi Kuu England
2021-01-14 18:27:26| cri

Timu ya Sheffield United, juzi ilifanikiwa kupata ushindi wake wa kwanza kwenye Ligi Kuu England baada ya kuwachapa Newcastle United bao 1-0. Katika michezo yake 17 iliyopita, vijana hao walifanikiwa kupata sare kwenye michezo miwili, wakipoteza michezo 15 kabla ya ushindi katika mchezo wa 18 Katika michezo yote hiyo, walikuwa wamefunga mabao manane tu na hili la juzi la tisa na kufungwa mabao 29. Bao la pekee kwenye mchezo huo lilifungwa na Billy Sharp kwa mkwaju wa penalti jambo ambalo liliwafanya washangilie sana mwishoni mwa mchezo huo. Wachezaji wa timu hiyo walionekana wakishangilia kama vile wametwaa ubingwa na hata kwenye vyumba waliendelea kushangilia kuonesha kuwa ni ushindi ambao wameusubiri kwa muda mrefu.