Bei za nafaka kaika masoko mbalimbali nchini Tanzania zimepungua kwa asilimia tano ,huku bei ya viazi mviringo na mazao ya viungo na matunda zikiongezeka hadi asilimia 12.
Kwa mujibu wa taarifa ya wiki ya mwenendo wa bei za mazao ya chakula iliyotolewa na Wizara ya Kilimo, Sehemu ya Masoko ya Mazao ya Kilimo, bei hizo zimebadilika kati ya Desemba mwaka jana na Januari 8, mwaka huu.
Katika mwenendo huo, wastani wa bei za mahindi na mtama kitaifa hazijabadilika, ambapo kuanzia Desemba 28, mwaka jana gunia la kilo 100 limeendelea kuuzwa kwa Sh 57,000 hadi kufikia Januari 8, mwaka huu.
Aidha, gunia la mtama la kilo 100 limeendelea kuuzwa kwa Sh 88,000 kwa kipindi hicho, wakati maharage na mchele bei zimepungua kwa asilimia tano na bei ya viazi mviringo ikiongezeka kwa asilimia sita.
Bei ya mchele hivi sasa gunia la kilo 100 linauzwa kwa wastani wa Sh 141,350 kutoka wastani wa Sh 149,000 katika mikoa mingi isipokuwa maeneo ya Mpanda (Katavi) na Musoma (Mara) ambako bei ya gunia moja ni wastani wa Sh 96,000.
Kwa zao la maharage, gunia la kilo 100 hivi sasa linauzwa kwa wastani wa Sh 197,000 kutoka Sh 207,000 Desemba mwaka jana, lakini mkoani Dar es Salaam bei ya zao hilo katika soko la Tandika imeendelea kubaki ile ile ya Sh 260,000 kwa gunia la ujazo huo tangu Desemba 21, mwaka jana.