SOKA: Cristiano Ronaldo awa miongoni mwa wanasoka wanaoshikilia rekodi ya mfungaji bora wa muda wote duniani
2021-01-14 18:28:09| cri

Cristiano Ronaldo kwa sasa ni miongoni mwa wanasoka wanaoshikilia rekodi ya mfungaji bora wa muda wote duniani baada ya kupachika wavuni goli lake la 759 kitaaluma kwenye ushindi wa 3-1 uliosajiliwa na waajiri wake Juventus dhidi ya Sassuolo mnamo Januari 11, 2021.

Akivalia jezi za Sporting Lisbon nchini Ureno, Ronaldo alipachika wavuni mabao matano kabla ya kufunga mengine 450 akiwa mchezaji wa Manchester United. Kabla ya kutua Juventus ambao kwa sasa amewafungia magoli 84, fowadi huyo alikuwa amewafungia Real Madrid magoli 450. Kufikia sasa, ametikisa nyavu za wapinzani mara 102 akiwajibikia timu yake ya taifa ya Ureno.

Hata hivyo, kwa mujibu wa takwimu za mtandao wa Rec.Sport.Soccer Statistics Foundation (RSSSF), Josef Bican ndiye mfungaji bora wa muda wote (ukiondoa wachezaji ambao hawajawahi kucheza soka ya haiba kubwa) baada ya kufunga jumla ya mabao 805 kutokana na mechi 530.

Romario anafuata kwa mabao 772 akifuatwa na Pele aliyefunga magoli 767 katika enzi yake ya usogora.

Bican, ambaye aliaga dunia mnamo 2001, alichechezea vikosi vitano tofauti vikiwemo Rapid Vienna, Slavia Prague, Czechoslovakia na Austria kati ya 1931 na 1955.