Biashara kati ya China na Misri yaongezeka japo dunia inakabiliwa na janga la COVID-19
2021-01-15 16:59:42| CRI

Kansela wa uchumi wa ubalozi wa China nchini Misri Han Bing ameitisha mkutano na waandishi wa habari kwa njia ya mtandao wa Internet, ili kueleza hali ya ushirikiano wa uchumi na biashara kati ya nchi hizo mbili katika mwaka uliopita. Amesema biashara kati ya China  na Misri imeongezeka kwa utulivu japo dunia inakabiliwa na changamoto ya janga la COVID-19.

Han amesema, biashara kati ya China na Misri imeongezeka kwa utulivu, na mwaka 2020 China iliendelea kuwa mwenzi mkubwa zaidi wa kibishara wa Misri. Anasema,

“Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na forodha ya China, katika miezi 11 ya mwanzo ya mwaka uliopita, thamani ya biashara kati ya China na Misri ilifikia takriban bilioni 12.9 za kimarekani, ambalo ni ongezeko la asilimia 10 ikilinganishwa na mwaka 2019 kipindi kama hiki.”

Han amesema serikali ya China inajitahidi kufungua soko kwa mazao ya kilimo ya Misri, ili kuhimiza biashara kati yao iendelee kwa uwiano. Hadi sasa aina kadhaa za matunda na mboga za Misri zimefanikiwa kuingia kwenye soko la China, na Misri imekuwa nchi ya kwanza inayoruhusiwa kuuza tende mbichi nchini China, huku machungwa yake yakichukua asilimia 20 ya soko la China.

Aidha, Han amesema mwaka uliopita China na Misri zilishirikiana vizuri katika kukabiliana na janga la COVID-19. Nchi hizo mbili zimesaini makubaliano ya ushirikiano wa chanjo ya virusi vya corona, na kampuni za China pia zimeanzisha viwanda vya kuzalisha barakoa nchini Misri. Han anasema,

“Ingawa tumekabiliwa na changamoto ya janga la COVID-19, lakini uwekezaji wa kampuni za China nchini Misri haukusita, badala yake, umeongezeka kwa kiasi kikubwa.”

Takwimu zinaonesha kuwa kuanzia mwezi Januari hadi Septemba mwaka 2020, uwekezaji wa moja kwa moja wa China nchini Misri uliongezeka kwa karibu dola milioni 90, ambalo ni ongezeko la asilimia 19.3 ikilinganishwa na mwaka 2019 kipindi kama hiki. Baada ya ujenzi wa miaka 12, Eneo la Ushirikiano wa Uchumi na Biashara kati ya China na Misri la TEDA Suez limekuwa eneo kubwa zaidi la viwanda nchini Misri, na hadi mwishoni mwa mwaka uliopita, limevutia kampuni 96, na kuleta ajira takriban 4,000.

Han amesema kutokana na juhudi kubwa, miradi ya ujenzi iliyotekelezwa na kampuni za China nchini Misri haikuathiriwa sana na janga la COVID-19, na baadaye kampuni za China zitaendelea kushiriki kwenye ujenzi wa miundombinu nchini Misri, ili kupanua mafanikio ya ushirikiano halisi kati ya nchi hizo mbili.