Tanzania yapigia debe utaratibu wa mafunzo ya kilimo, mifugo kwa vijana
2021-01-15 19:23:39| cri

Serikali ya Tanzania imeombwa kuandaa utaratibu wa kutoa mafunzo ya kilimo na ufugaji kwa wanafunzi wa vyuo, ili kuwaandaa kujiajiri wenyewe wanapohitimu masomo yao.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya Glaring Future Foundation (GFF), Mhandisi Aisha Msantu, alisema kuna umuhimu wa kutoa mafunzo hayo kwa vijana wa vyuo ili kuchangamkia fursa zilizopo kwenye sekta ya kilimo na ufugaji ambazo zitawasaidia kujiajiri badala ya kusubiri kuajiriwa na serikali.

Msantu alisema baadhi ya vijana hawana uelewa kuhusu sekta hizo zinavyochangia ukuaji wa uchumi hivyo ni vyema serikali ikawa na utaratibu wa kuendesha semina endelevu ambazo zitasaidia kuwajenga uwezo kwenye nyanja hizo. Pia alisema warsha zikiwa zinafanyika mara kwa mara hizo zitasaidia kufikisha fursa ambazo baadhi yao hawajui.

Alisema lengo lao ni kuona vijana wanatumia fursa zilizopo ili kuhakikisha wanachangia kukuza uchumi wa kati wa viwanda.

Hata hivyo, alisema taasisi hiyo imejipanga kuhakikisha vijana wanatumia fursa hizo na kuchangia pato la taifa.