Makamu Rais ahimiza ushirikiano na sekta binafsi kuleta maendeleo
2021-01-15 19:23:14| cri

Serikali ya Zanzibar imesema fursa nyingi zinazopatikana ndani ya sekta binafsi zinaweza kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi kwa taifa endapo zitatumiwa vizuri.

Akizungumza na viongozi wa Bodi ya Jumuiya ya Kitaifa ya Wafanyabiashara, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema sekta binafsi ina mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa na ustawi wa wananchi katika maeneo mbalimbali.

Hemed alisema kwa vile sekta binafsi inaweza kufanya vyema katika ajira, serikali imejikita kufanya kazi kwa karibu na sekta hiyo kupitia Jumuiya ya  Wafanyabiashara ili kuona malengo ya pande zote mbili katika ongezeko la mapato yanafanikiwa.

Aliupongeza uongozi wa bodi hiyo kwa mtazamo wake wa kwenda sambamba na kasi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, jambo ambalo limeanza kuleta faraja hasa kitendo cha kuanza kwa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa.

Hemed aliutaka uongozi huo ufanyie marekebisho na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya washirika wa biashara.

Aliwakumbusha viongozi wa bodi hiyo kuendelea kutoa elimu kuhusu umuhimu wa wafanyabiashara kulipa kodi jambo ambalo halina mjadala kwa vile ni wajibu wao kufanya hivyo.