Ni haki kufanya wanawake wachague moja kati ya elimu au ndoa?
2021-01-21 19:51:37| cri

Nchini China kuna msemo mmoja maarufu, lakini wanawake hawaupendi sana. Kwa kiingereza ni "leftover women" yaani “wanawake makombo”. Hii ina maana wanawake wenye umri wa zaidi ya miaka 30 na bado hawajaolewa. Mwaka hadi mwaka idadi ya wanawake hao imeendelea kuongezeka, na kadiri mwanamke anavyokuwa na elimu zaidi, ndivyo uwezekano wa kukosa kuolewa unaongezeka. Mwaka 1990 kulikuwa na wanawake 460,000 wenye umri wa miaka 30 na zaidi wasioolewa nchini China. Mwaka 2000 idadi hiyo iliongezeka na kuwa zaidi ya milioni 1.54, na mwaka 2015 ilipanda hadi milioni 5.9. Kiwango cha ndoa cha China kimeendelea kupungua tangu 2013, lakini kiwango cha talaka kimeendelea kuongezeka. Kuanzia 2013 hadi 2019, idadi ya ndoa zilizosajiliwa nchini China ilipungua kutoka asilimia 99 hadi asilimia 66.

 

Watu wengi wanaamini kuwa uhuru wa wanawake kiuchumi na kuongezeka kwa kiwango cha elimu kwa wanawake ni moja ya sababu zinazochangia wanawake kutoolewa mapema au hata kutoolewa kabisa. Takwimu zinaonyesha kuwa kiwango cha wasioolewa cha wanawake wenye elimu ya shahada ya chuo Kikuu walio na zaidi ya miaka 30 ni asilimia 11.

 

Hali hii ya China pia inalingana na dhana ya Afrika ya kale. Zamani wanawake hawakutakiwa kupata elimu ya juu, walitakiwa kuwa na elimu ya msingi tu na wanapoanza maisha ya ndoa walikuwa mama wa nyumbani. Lakini kutokana na shinikizo la maisha na maisha kuanza kuwa magumu, wanaume wengi walianza kupungukiwa na mapato ya kukidhi mahitaji yote ya familia. Wanawake wengi siki hizi pia hawapendi dhana ya kuitwa tegemezi au jina baya la kuitwa “golikipa”. Hali hizo ziliwalazimu wanawake kuanza kufanya biashara ndogondogo na kuongeza elimu na kuchuma pesa ili kusaidia waume wao. Lakini wanaume wengi hasa wale waliozaliwa kwenye miaka ya 80 na 90 wanaona mwanamke mwenye elimu na pesa ni vigumu kumdhibiti, na sababu hii inawafanya wanawake wengi wasiolewe.

 

Changamoto iliyopo ni kuwa, muda wa elimu huchelewesha muda wa wanawake kuingia kwenye ndoa. Na elimu yenyewe hupunguza nafasi ya wanawake kuolewa. Lakini swali lililopo ni kuwa kwenye mazingira na muktadha huu, ni haki kwa wanawake kulazimika kuchagua moja kati ya ndoa na elimu?