Majukwaa ya malipo Uganda yatarajia kuboreka baada ya shule kufunguliwa
2021-01-21 20:05:21| cri

Wadau katika sekta ya majukwaa ya malipo nchini Uganda wanasema kuwa ufunguaji wa shule nchini humo utaleta maboresho katika miamala ya ulipaji ada mwaka huu.

Ufungwaji wa shule uliosababishwa na janga la korona ulifanya majukwaa mengi ya malipo kutotumika,hivyo basi kusababisha kushuka kwa mapato.

Athari ya Covid-19 imeonekana mno katika jukwaa la ulipaji la School Pay,ambalo linatumiwa na benki 15 na shule zaidi ya 15,000.

Meneja wa jukwaa la malipo la School Pay,Bw Osbert Muganga amesema kuwa mwaka 2009 walikusanya Sh700b.Katika robo ya kwanza ya mwaka 2020 walikusanya takriban Sh200b,na baada ya amri ya kutotoka nje kufuatia janga la corona,wamekusanya Sh70b.

Takriban asilimia 90 ya miamala hukamilishwa kupitia simu za mkononi huku mabenki yakichukua asilimia 10.

Kabla ya Covid-19,wazazi milioni 3 walilipa ada ya shule kupitia School Pay.

Hata hivyo,idadi hiyo ilikuwa chini na kuanza kufufuka kiasi mwezi Oktoba mwaka jana baada ya serikali kufungua shule.

Kulingana na Muganga,malipo yaliongezeka kutoka sifuri hadi wazazi 185,000.