Kocha msaidizi wa Yanga atangaza kujiuzulu kwa sababu za kiafya
2021-01-22 19:13:17| cri

Kocha msaidizi wa klabu ya Yanga, Juma Mwambusi amejiondoa kwenye kuifundisha Yanga kwa kile alichokieleza kuwa ni sababu za kiafya. Mwenyekiti wa klabu, Dk Mshindo Msolla amethibitisha kujiuzulu kwa Mwambusi aliyekuwa anafanya kazi kwa awamu ya pili Yanga baada ya awali kufanya kazi chini ya kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm na Mzambia, George Lwandamina. Dk. Msolla amesema watazungumza na kocha Mkuu, Mrundi Cedric Kaze kupata maoni yake juu ya msaidizi mpya amtakaye. Tayari kuna tetesi kwamba kiungo wa zamani wa klabu hiyo, Nizar Khalfan ndiye atakayechukua nafasi hiyo kwa sababu ndiye chaguo la Kaze. Wakati Kaze alikuwa anafundisha akademi ya Barcelona nchini Canada, Nizar Khalfan alikuwa anachezea timu ya Vancouver Whitecaps ya nchini humo, ambayo ilikuwa inashiriki Ligi Kuu ya huko. Mwambusi ndiye kocha aliyekiandaa kikosi cha Yanga kwa ajili ya msimu huu kabla ya kuletwa Mserbia, Zlatko Krmpotic aliyedumu kwa mwezi mmoja tu na kuondolewa akimpisha Kaze.