Burkina Faso yaitoa Zimbabwe kombe la CHAN, Uganda na Rwanda uwanjani leo
2021-01-22 19:14:35| cri

Wenyeji Cameroon watahitaji kushinda mechi ngumu ya mwisho dhidi ya Burkina Faso ili kwenda Robo Fainali ya Michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Mali jana. Cameroon ilikuwa ya kwanza kufunga goli katika dakika ya sita lakini Mali ilisawazisha katika dakika ya 12. Burkina Faso imepata ushindi wa kwanza, baada ya kuichapa Zimbabwe 3-1. Cameroon inaendelea kuongoza Kundi A kwa pointi zake nne sawa na Mali, ikifuatiwa na Burkina Faso yenye pointi tatu, wakati Zimbabwe inakuwa timu ya kwanza kuaga mashindano baada ya kufungwa mechi zote mbili za kwanza. Kwenye kundi D ilipo timu ya Tanzania, kesho tutajua nani anaaga mashindano hayo, kwani Namibia iliyofungwa na Guinea sasa iko mkiani na pointi 0, huku Guinea na Zambia zikiwa juu na point tatu. Timu nyingine za Afrika Mashariki ni Rwanda ambayo leo inacheza na Morocco, na Uganda itakutana na Togo. Rwanda na Uganda haziko pabaya kwa kuwa zina pointi moja. Mpaka sasa ni timu ya DRC kutoka kwenye eneo la Afrika Mashariki ndio inaongoza kundi lake na iko kwenye nafasi nzuri ya kusonga mbele.