Huduma ya Kuagiza Chakula cha Asubuhi Mtandaoni
2021-01-22 16:53:36| cri

Katika jengo moja la ofisi wilayani Huangpu mjini Shanghai, duka moja la kifungua kinywa ambalo wateja wanaweza kuagiza chakula mapema kwa njia ya mtandao na halafu kukichukua wenyewe kutoka kwenye makabati yaliyoko nje ya duka hilo, ni la kwanza la aina yake mjini Shanghai.

Wateja wanaweza kuweka oda kupitia App ya simu ya mkononi, na baada ya dakika mbili tu watapokea Password ya kuchukua chakula chao kutoka kwenye makabati.

Maduka kama hayo yamesanifiwa kwa ajili ya wafanyakazi wa ofisini, na mengi yako njiani kwao kwenda kazini. Wateja wanaweza kutumia Yuan kumi hivi kununua vyakula mbalimbali ikiwemo kahawa, maziwa ya soya, mkate na maandazi ya kichina.

Mmiliki wa duka hilo lililofunguliwa mwezi Julai mwaka jana alisema duka lake limeanza kupata faida kuanzia mwezi Juni mwaka huu, hivi sasa wanaweza kupata oda 700 hadi 800 kila siku, na thamani ya mauzo inaweza kufikia yuan elfu saba kwa siku.