TARI kuongeza uzalishaji mbegu bora za mkonge Tanzania
2021-01-22 18:29:31| cri

Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), inakusudia kuzalisha mbegu bora ya mkonge  kutoka miche milioni 2.5 ya sasa kufikia milioni 10 kwa mwaka itakayozalishwa kwa njia ya chupa.

Uzalishaji huo unalenga kukidhi mahitaji ya soko la  dunia la mkonge la takriban tani 500,000 kwa mwaka wakati uzalishaji kwa sasa ni tani 280,000, huku  Tanzania ikiwa ya pili kwa uzalishaji huo ikizalisha wastani wa tani 40,000 kiasi ambacho ni kidogo ukilinganisha na fursa iliyopo ya uzalishaji.

Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dk. Geofrey Mkamilo, alisema uzalishaji wa mbegu bora za mkonge unafanywa kwa kutumia vikonyo ambao unazalisha miche milioni 2.5 kwa mwaka hivyo maabara ya Tissue Culture itakapofanyiwa ukarabati wa kina itaongeza na kufikia milioni 10, hivyo kukidhi mahitaji ya mbegu kwa wakulima wa mikoa yote inayolima mkonge.