Ujenzi wa bandari mpya eneo la Shimoni kaunti ya Kwale inayokadiriwa kugharimu Sh20 bilioni unaweza kuendelea bila pingamizi baada ya wawekezaji kukubaliana kuhusu masuala tata.
Hata hivyo, Halmashauri ya Bandari za Kenya nchini (KPA) imetakiwa kushughulikia masuala mengine ambayo yanahusiana na uharibifu wa mazingira.
Ujenzi wa bandari hiyo utabadilisha mandhari ya Kwale, hasa uchumi wa baharini.
Gavana wa Kwale Salim Mvurya alisema ujenzi wa bandari hiyo karibu na mpaka wa Kenya na Tanzania utapiga jeki uchumi wa eneo hilo mbali na kuwapa vijana ajira.
Aidha Gavana Mvurya aliwahimiza vijana kupata ujuzi wa kiufundi ili kufaidika kutokana na nafasi za kazi ambazo zitapatikana kupitia kwa mradi huo.