SOKA: CAF yatoa maamuzi mechi ya Namungo FC na Waangola
2021-02-17 16:13:39| CRI

Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeamua mechi zote mbili za Kombe la Shirikisho kati ya CD 1 Agosto ya Angola na Namungo FC ya Tanzania zichezwe nchini Tanzania. Uamuzi huo umefanywa baada ya Kamati ya CAF ya Mashindano hayo kubaini kuwa si Agosto wala Namungo iliyohusika moja kwa moja kukwamisha mechi ya kwanza iliyokuwa ichezwe Februari 14 nchini Angola. Mechi zote mbili zinatakiwa kuchezwa angalau ndani ya saa 72, na ziwe zimechezwa kufikia Februari 26 mwaka huu. Kwa mujibu wa ratiba, CD 1 Agosto itakuwa mwenyeji wa mechi ya kwanza, hivyo itawajibika katika maandalizi yote ikiwemo gharama za maofisa wa mechi hiyo.