CAF yaamua mechi zote mbili za Namungo na Primiero de Agosto zichezwe Tanzania ndani ya saa 72
2021-02-18 15:28:06| cri

Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limeamua mechi zote mbili za Kombe la Shirikisho kati ya Primiero de Agosto ya Angola  na Namungo FC ya Tanzania zichezwe nchini Tanzania. Uamuzi huo umefanywa baada ya Kamati ya CAF ya Mashindano hayo kubaini kuwa si Agosto wala Namungo iliyohusika moja kwa moja kukwamisha mechi ya kwanza iliyokuwa ichezwe Februari 14 nchini Angola. Mechi zote mbili zinatakiwa kuchezwa angalau ndani ya saa 72, na ziwe zimechezwa kufikia Februari 26 mwaka huu. Kwa mujibu wa ratiba, Primiero de Agosto ya Angola itakuwa mwenyeji wa mechi ya kwanza, hivyo itawajibika katika maandalizi yote ikiwemo gharama za maofisa wa mechi hiyo. Kwa vile makundi ya Kombe la Shirikisho yatapangwa Februari 22, mshindi wa jumla baada ya mechi hizo mbili hatazingatiwa katika viwango (non-ranked) wakati wa upangaji.