Mzee ahukumiwa kifungo kwa kuongeza kasi gari lake na kusababisha kifo cha mtu asiyejulikana ambaye alipanda juu ya gari lake barabarani
2021-02-18 15:45:00| cri

Baada ya kugombana na mke wake, kijana Li kutoka mji wa Weifang mkoani Shandong alitoka nyumbani na kuingia barabarani, akijaribu kuzuia gari moja baada ya jingine, hatimaye akafanikiwa kusimamisha gari la mzee Li Jixiao mwenye umri wa zaidi ya miaka 60, halafu akapanda juu ya gari lake.

Mzee huyo alisema kuwa wakati ule aliogopa kuwa atashambuliwa na kijana huyo ambaye alipanda ghafla juu ya gari lake, kwa hivyo hakuthubutu kutoka garini na badala yake aliongeza kasi ili kupita lori dogo lililosimama mbele ya gari lake.

Baada ya gari hilo kuenda mbele kidogo, kijana Li alianguka kutoka juu ya paa la gari hilo na kupoteza fahamu. Shuhuda mmoja alisema kuwa wakati tukio hilo lilipotokea, kijana huyo alipoteza kabisa uwezo wa kujidhibiti, na alikuwa anaonekana kama “mwenda wazimu”.

Kijana huyo alikimbizwa hospitali na kufariki dunia siku tano baadaye.

Miezi minane baada ya kutokea tukio hilo, Mzee Li Jixiao alifunguliwa mashtaka mahakamani, na Oktoba 29 mwaka jana, mzee huyo alihukumiwa kifungo cha miaka miwili na nusu jela kwa kosa la kuua bila ya kukusudia, na pia alitakiwa kulipa fidia ya yuan laki 1.18 kwa familia ya muhanga.

Baada ya hukumu hiyo kutolewa, Mzee Li Jixiao alikata rufaa na kudai kuwa kitendo chake kilikuwa cha kujilinda wakati alipokabiliwa na tishio la ghalfa lilifanywa kwa makusudi na muhanga huyo.

Mpaka sasa mahakama ya rufaa bado haijatoa uamuzi juu ya kesi hiyo.