Tanzania-Posta yapanua mtandao wake wa kufanya baishara
2021-02-18 19:57:18| cri

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile amesema Shirika la Posta Tanzania (TPC) lipo katika mkakati wa kujiingiza zaidi katika biashara mtandao kwa sababu Shirika hilo lina faida ya kuwa na mtandao mpana ndani ya nchi na kuunganishwa na matawi mbalimbali ya posta yaliyopo katika nchi  nyingine.

Dkt. Ndugulile amezungumza hayo alipotembelewa ofisini kwake na Katibu Mkuu wa Umoja wa Posta Afrika (PAPU) Younouss Djibrine kwa ajili ya kufahamiana na kuzungumzia taarifa za mafanikio na kubadilishana mawazo kuhusu huduma za posta katika bara la Afrika.

Aliongeza kuwa kuna mabadiliko makubwa katika utoaji wa huduma za posta nchini ambapo kwa sasa Shirika hilo limejikita kwenye usafirishaji wa vifurushi na vipeto, biashara ya kubadilisha fedha na biashara mtandao.

Naye Katibu Mkuu PAPU, Younouss Djibrine amesema kuwa huduma za posta zimeweza kutambuliwa duniani kuwa ni moja ya huduma muhimu hasa katika kipindi hiki cha mlipuko wa ugonjwa wa Korona ambapo Shirika hilo limekuwa likifikisha vifurushi hadi mlangoni, kutoa huduma za kifedha na sasa limeanza kuwa kituo cha kutoa huduma jumuishi.