Serikali kuongeza uwekezaji kwenye visiwa vidogo Zanzibar
2021-02-18 19:58:12| cri

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mudrik Ramadhani Soraga, amesema uwekezaji katika visiwa vidogo vidogo vya Zanzibar ukisimamiwa vizuri unaweza kuwa chachu ya uchumi wa nchi.

Soraga alisema hayo wakati alipofanya ziara katika kisiwa cha Mnemba, mkoa wa Kaskazini Unguja, wakati kuangalia uwekezaji unaoendelea katika kisiwa hicho.

Alisema serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, imeandaa mpango madhubuti kuendeleza uwekezaji wa visiwa hivyo ili uwekezaji wake uwe na tija kwa serikali.

Alisema kisiwa cha Mnemba ni kisiwa kizuri kwa uwekezaji lakini kina mchango mdogo kwenye mapato ya serikali ikilinganishwa na mapato anayoyapata muwekezaji kwenye kisiwa hicho hivyo aliwataka wawekezaji kuupokea mpango huo kwa maslahi ya nchi.