Ustawi wa soko la matumizi wakati wa Sikukuu ya Spring waonesha uhai na mustakabali mzuri wa uchumi wa China
2021-02-18 17:15:38| cri

Ustawi wa soko la matumizi wakati wa Sikukuu ya Spring waonesha uhai na mustakabali mzuri wa uchumi wa China_fororder_1127110982_16136349348691n

Watu wengi wamesherehekea Sikukuu ya Spring ambayo ni mwaka huu mpya wa jadi wa China katika maeneo waliyopo bila ya kurejea kwenye maskani zao kama ilivyo desturi. Watu hao walifanya manunuzi kupitia mtandao wa internet na kutembelea sehemu za pembezoni mwa miji waliyomo, hali iliyochea soko la matumizi.

Wakati wa sikukuu ya Spring, filamu nyingi zilizotengenezwa China zimeoneshwa na kustawisha soko la filamu. Mameneja wa majumba mbalimbali ya filamu wanasema:“Watazamaji wetu wengi ni vijana na wanafunzi, na wale wanaotazama filamu kwa familia. Mapato ya mauzo ya tiketi yamefikia dola za kimarekani elfu 30, ambayo yamezidi tulivyotarajia.”

Ustawi wa soko la filamu vilevile umeonesha ustawi wa soko la matumizi nchini wakati wa sikukuu ya Spring kwa mwaka huu. Takwimu zimeonesha kuwa, wakati wa sikukuu hiyo, thamani ya mauzo ya makampuni makubwa ya bidhaa za rejareja na vyakula nchini imezidi dola za kimarekani bilioni 120, thamani ya mauzo ya bidhaa za rejareja kupitia mtandao wa Internet imezidi dola za kimarekani bilioni 18.5, huku idadi ya vifurushi vilivyosambazwa ikizidi milioni 480, ikiwa ni mara tatu zaidi ya mwaka jana wakati kama huu.

Masanduku ya zawadi, mitambo ya umeme ya nyumbani, na vifaa vya kujenga afya viliuzwa kwa kiasi kikubwa, huku ongezeko la mauzo ya vito, nguo, na vipodozi ikizidi asilimia 100, mauzo ya maua, vito vya dhahabu zikiongezeka kwa kiasi kikubwa.

Mkurugenzi wa Taasisi ya biashara ya kimataifa na ushirikiano wa kiuchumi katika Wizara ya Biashara Gu Xueming anaona kuwa, kupanuka kwa soko la matumizi kumeweka msingi imara wa kujenga muundo mpya wa maendeleo ambao unachukua mzunguko wa ndani kuwa nguzo na kuinua mizunguko miwili ya ndani na ya kimataifa. Anasema:“Ongezeko kubwa la matumizi wakati wa Sikukuu ya Spring, limeonesha mustakabali mzuri wa China kuhimiza matumizi, na kupanua mahitaji ya ndani. Soko kubwa la ndani na kuboreshwa kwa muundo wa matumizi ni sifa ya maendeleo ya uchumi wa China.”