ZFF yasimamisha michezo yote ya soka visiwani kutokana na kifo cha Maalim Seif Sharif Hamad
2021-02-18 15:29:03| cri

Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF) limesimamisha michezo yote ya soka visiwani kutokana na kifo cha Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad. Mjumbe wa Bodi ya Ligi ya ZFF, Muhammed Masoud amesema ligi hizo zitasimama mpaka watakapo pata maelekezo kutoka serikalini. Masoud amesema ligi ambazo zilikuwa zikiendelea kwa sasa kwa ngazi ya taifa ni Ligi Daraja la Kwanza pamoja na michuano ya Kombe la Shirikisho (FA Cup). Ambapo leo Alhamisi kwa mujibu wa ratiba kulikuwa kufanyike michezo miwili ya ligi daraja la kwanza kati ya timu ya Mchangani waliokuwa wacheze na Idumu kwenye Uwanja wa Mao Tse Tung, huku mchezo mwingine ulikuwa kati ya Jang'ombe Boys na Muembe Makumbi uliokuwa ufanyike kwenye Uwanja wa Amaan. Amesema kwa sasa ligi mbili tu ndizo zilizoathirika, ila ikiwa wataambiwa wasubiri hadi zimalize siku saba za maombolezo basi na Ligi Kuu nayo itaathirika kwani ilikuwa inatarajiwa kuanza duru ya pili Febuari 20. Hata hivyo ameomba wadau wa soka visiwani kuwa na moyo wa subra katika kipindi hichi kigumu.