Watu 7 wauawa kwenye ajali ya ndege ya jeshi la Nigeria
2021-02-22 09:05:38| CRI

Watu 7 wameuawa baada ya ndege ya jeshi la Nigeria kuanguka mjini Abuja.

Msemaji wa jeshi la anga la Nigeria Bw. Ibinkunle Daramola, amesema ndege hiyo aina ya Beechcraft KingAir B350i ilianguka wakati inarudi kwenye uwanja wa ndege wa Abuja, baada ya kukumbwa na hitilafu ya injini ikiwa inaelekea katika mji wa Minna. Watu wote saba waliokuwa kwenye ndege hiyo walikufa kwenye ajali hiyo.

Mkuu wa jeshi la anga la nchi hiyo Oladayo Amao ameagiza uchunguzi ufanyike mara moja kuhusu ajali hiyo, na kutaka watu watulie kusubiri matokeo ya uchunguzi huo.

Taarifa za awali kutoka idara ya uchunguzi wa ajali ya Nigeria (AIB) zinasema kisanduku cha kurekodi sauti kimepatikana. Rubani wa ndege hiyo hakutoa taarifa ya hatari, kwa kuwa alidhani anaweza kutua salama alipokuwa umbali wa mita 400 kutoka uwanjani.