ZANZIBAR: WATAALAM KILIMO WASHAURIWA KUANZINSHA MASHAMBA DARASA
2021-02-22 16:56:42| cri

Wataalam wa Kilimo Kisiwani Pemba,  wametakiwa  kuanzisha mashamba darasa kwa wakulima, ili kutoa fursa ya kujifunza mbinu mpya za kilimo chenye tija na kuleta mabadiliko chanya ya kilimo katika maeneo yao.

Katibu Tawala Wilaya Ndogo Kojani, Makame Khamis Makame, aliwasisitiza wataalamu hao wa kilimo kutumia taaluma yao kufanya utafiti wa udongo hali itakayo wawezesha wakulima  kutambua aina ya udongo  sambamba na aina ya mbegu lengo ni kuongeza uzalishaji.

Hayo aliyasema wakati akifunga mafunzo ya siku tano ya  kilimo cha Viungo , Mboga Mboga na Matunda kwa mabwana na mabibi shamba kisiwani Pemba,

Alisema kutokana na changamoto hiyo wakulima wengi wanalima bila ya kuwa na taaluma sahihi ya kutumia mbegu zinazoendana na udongo na hivyo kusababisha kukosa tija kwa kilimo. Meneja wa mradi wa viungo, mboga mboga na matunda, Sharif Maalim Hamad, amesema wanatarajia kuwanufaisha wakulima 21,000 Unguja na Pemba huku wengi wao na wanawake.

Aidha aliwataka mabwana na mabibi shamba kuhakikisha wanawake wanashiriki kwa wingi katika mashamba darasa ili kutoa fursa ya kupata taaluma za kilimo.

Washiriki wa mafunzo hayo wameahidi kutamia mafunzo hayo kuimarisha mashamba darasa ambayo ni sehemu sahihi ya wakulima kupata taaluma ya kilimo.

Mradi huo pia ni suluhisho ya changamoto ya soko la bidhaa za zitokanazo la mboga mboga,viungo pamoja na matunda.