China yapongezwa kwa kuhimiza upatikanaji wa haki wa chanjo ya COVID-19
2021-02-22 09:53:48| CRI

 

 

Gazeti la The People la Kenya limetoa tahariri ikiipongeza China kwa kuhimiza upatikanaji wa haki wa chanjo ya COVID-19 kwa hatua halisi.

Tahariri hiyo inasema, janga la COVID-19 limeleta changamoto kubwa duniani, ikiwemo kukatishwa kwa safari za kuvuka mpaka, kudidimia kwa uchumi wa dunia, kufufuka kwa umwamba wa kisiasa na mawazo ya vita baridi, na ongezeko la vitendo vya upande mmoja na kujilinda. Baadhi ya nchi zinalichukua janga hilo kama suala la kisiasa, kukataa sayansi, kuchochea ubaguzi, kueneza habari za uwongo, na kupuuza mahitaji ya nchi zinazoendelea. Takwimu zilizotolewa na Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa, nchi 10 zimedhibiti asilimia 75 ya chanjo ya COVID-19 duniani. Wakati huohuo, China imetoa misaada ya chanjo hiyo kwa nchi 53 zinazoendelea duniani, na kuiuza kwa nchi 22. Pia imeahidi kutoa dozi milioni 10 kwa Mpango wa Kimataifa wa Chanjo ya COVID-19 (COVAX), ili kukidhi mahitaji ya haraka ya nchi zinazoendelea.

Tahariri hiyo inasisitiza kuwa, pande mbalimbali duniani zinapaswa kushirikiana kupinga “utaifa wa chanjo”, ili kuhimiza upatikanaji wa haki wa chanjo ya COVID-19 kwa gharama nafuu kwa nchi zote duniani, zikiwemo nchi zinazoendelea, na haswa zile zenye migogoro.