Mradi wa usambazaji gesi majumbani Sinza kukamilika ndani ya miezi sita
2021-02-22 16:55:31| cri

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC limesema mradi wa usambazaji wa gesi asilia majumbani katika nyumba 506 ndani ya Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, umeanza kwa kasi na utakamilika baada ya miezi sita.

Hayo yamebainisha mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dk. James Mataragio, mara baada ya kufanya ziara ya kujionea utekelezaji wa maagizo ya waziri wa Nishati,(Dk. Medard Kalemani) aliyemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi huo ambayo ni Kampuni ya BQ kukamilisha mradi huo ndani  ya muda mfupi  na si mwaka  mmoja kama ulivopangwa.

Dk.Mataragio amesema, baadhi ya changamoto ambazo zingechelewesha mradi huo zimeshapatiwa ufumbuzi na kufafanua kuwa mradi huo ungetumia mwaka mmoja kutokana na uagizaji wa vifaa nje ya nchi kutumia muda wa takribani miezi sita mpaka kufika nchini.

Dk.Mataragio ameongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutawezesha nyumba zaidi ya 500 zitanufaika na matumizi ya nishati hiyo ya gesi asilia.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya BQ, Mhandisi John Buza, amesema changamoto kubwa waliyokumbana nayo katika utekelezaji wa mradi huo ni wafanyabiashara nchini kuwauzia vifaa vinavyohitajika katika utekelezaji wa mradi huo kwa  gharama kubwa tofauti na zinavyouzwa nje ya nchi.