Bei ya mahindi yashuka bei.
2021-02-22 16:55:56| cri

Huku wakulima wakiendelea kuumia kutokana na bei duni ya mahindi Kaskazini mwa Bonde la Ufa, raia na wafanyabiashara wadogo wanaendelea kunufaika kutokana na kujaa kwa mazao hayo sokoni.

Mahindi kutoka nchi jirani za Uganda na Tanzania yamejaa sokoni huku raia wakikosa kununua pakiti ya unga madukani na badala yake kununua mahindi kisha kupeleka kwa mtambo wa kusaga kwa kuwa ni gharama nafuu.

Kampuni za kusaga mahindi nazo zinaendelea kupata hasara na zimeonya kwamba bei ya kila gunia la mahindi itaendelea kushuka zaidi huku zikitishia kupunguza idadi ya wafanyakazi wao. Kwa sasa gunia la mahindi la kilo 90 linauzwa kwa Sh2,400 kutoka Sh2,800.

Wengi wa wakulima wanaharakisha kuyauza mahindi yao huku wakijiandaa kwa msimu wa upanzi ambao unanukia mwezi ujao.

Bei ya kila gunia la kilo 90 la mahindi lilikuwa limepanda hadi Sh3,000 wakati ambapo kampuni za kusaga mahindi na Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) zilikuwa ziking’ang’ania mahindi kutokana na hofu ya kupungua kwake sokoni. Hofu hiyo ilichangiwa na mavuno duni msimu uliopita.

NCPB ilikuwa ikinunua kila gunia la kilo 90 kwa Sh2,700 kutoka kwa bei ya awali ya Sh2,500 huku ikikabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa kampuni za kusaga mahindi ambazo zilikuwa zikinunua kwa Sh3,000 kutoka Sh2,700.

Hata hivyo, familia nyingi sasa zinaweza kumudu bei ya unga kutokana na kujaa kwa mahindi sokoni na wengi huhiari kujinunulia kisha kuyasaga kwa kuwa ni nafuu kuliko kununua madukani.