Serikali imewatoa hofu wananchi wa maeneo ya Longido na kuwataka wasiwe na hofu kufuatia nzige walioovamia wilayani humo wakitokea nchi jirani ya Kenya.
Hayo yamebainishwa na jana Februari 21, na Waziri wa Kilimo, Prof. Adolf Mkenda, baada ya kutembelea eneo la Longido ambalo limevamiwa na nzige na kuwa kuanzia leo ndege maalum itafanya kazi kupulizia viuatilifu kuua nzige hao.
Prof. Mkenda amesema wananchi wasiwe na hofu nzige wote watadhibitiwa kupitia wataalam wa Wizara ya Kilimo waliopo kwenye maeneo yote yenye dalili za uwepo wa wadudu hao.
Prof. Mkenda amesema nzige wa jangwani wana athari kubwa katika uzalishaji wa mazao ya chakula na malisho ya mifugo na kundi moja la nzige lina uwezo wa kuruka bila kutua kwa umbali wa kilometa 150 Kwa siku.
Aidha, nzige wana uwezo wa kula Sawa na uzito wake kwa siku ambapo kundi moja la nzige linaweza kuwa na wastani wa nzige milioni 40 kwenye eneo la kilometa moja za mraba alisema Waziri Mkenda .